Viongozi wa Pwani wamekosolewa kwa kulifumbia macho suala la ulanguzi wa dawa za kulevya lililosababisha vijana wengi kuangamia kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Kulingana na Mkereketwa wa masuala ya kisiasa mjini Malindi Athman Ali Said, viongozi hao wameshindwa kulizungumzia suala tata la Dawa za kulevya ambalo limekithiri katika eneo la Pwani.
Said alisema wakati wa ziara ya rais Ruto hapa Pwani, viongozi ambapo walichaguliwa kupigania maslahi ya jamii walionekana kukwepa kulizungumzia suala hilo na kuangazia masuala ya kisiasa na ajenda zao binafsi za siasa za uchaguzi mkuu ujao.
“Tulichokishuhudia wakati wa ziara ya rais hasa kaunti ya Kilifi ilikuwa ni ahadi na siasa za uchaguzi mkuu ujao, huku viongozi wa Pwani wanaotegemewa na wananchi kama wawakilishi wao wakiangazia maslahi yao. Hali hii haitakuwa rahisi kwa jinamizi la Mihadarati kukomeshwa katika ukanda wa Pwani”, alisema Said.
Kwa upande wake Mwanaharakati wa kupambana na Mihadarati kanda ya Pwani Famau Mohammed Famau alisema kuna haja ya viongozi wa Pwani kuliangazia kwa kina janga la Mihadarati ili likomeshwe.
“Ingekuwa ni vyema rais angegusia suala la dawa za kulevya na vile vile akatuoa muongozo kwa wale ambao wanapambana na madawa haya kwamba wafanye nini ili kuzuia madawa ya kulevya yasiendelee katika mji wetu wa Malindi na Kilifi kaunti”, alisema Fahamu
