Mkuu wa mawaziri nchini Musalia Mudavadi amewataka wakenya kuzingatia taratibu zilizotolewa na Wizara ya afya nchini kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Ebola katika nchi jirani ya Uganda.
Mudavadi amesema kwamba kama vile wakenya walivyofanya wakati wa janga la COVID-19, wanapaswa kuwa makini ili kuilinda nchi dhidi ya virusi vya Ebola.
Amesema kuwa ingawa hadi sasa hakuna kisa kilichoripotiwa nchini, uzembe unaweza kuliingiza taifa katika matatizo, akisisitiza kuzingatiwa kwa taratibu zote za kiafya zilizotolewa na Wizara ya Afya nchini dhidi ya virusi hivyo hatari na ambavyo vinasambaa kwa kasi.
Taasisi ya afya ya umoja wa afrika imesema nchi kumi za Afrika ziko katika hatari ya kuathiriwa na ugonjwa wa virusi vya Ebola, mbali na DRC na Uganda.
Kenya ilithibitisha kuwa visa vyote vinavyoshukiwa vya Ebola vilivyogunduliwa kupitia mfumo wake ulioimarishwa wa ufuatiliaji vilipatikana kuwa hasi, huku nchi ikiendelea kuimarisha uchunguzi mipakani na maandalizi ya dharura kufuatia mlipuko wa kikanda katika nchi jirani.
Waziri wa Afya nchini Aden Duale siku ya Ijumaa wiki jana alisema kuwa serikali imeongeza ufuatiliaji katika maeneo yote ya kuingia nchini lakini akawahakikishia wananchi kuwa hakuna maambukizi yaliyothibitishwa yaliyorekodiwa.
Taarifa ya Joseph Jira
