Mkasa wa moto katika shule ya Utumishi Girls Academy wasababisha vifo 16

Mkasa wa moto katika shule ya Utumishi Girls Academy wasababisha vifo 16

Serikali imethibitisha kwamba wanafunzi 16 wa shule ya upili ya wasichana ya Utumishi Girls Academy eneo la Gilgil kaunti ya Nakuru wameaga dunia na wengini 79 wakajeruhiwa kufuatia mkasa wa moto ulitokea katika shule hiyo.

Waziri wa Elimu nchini Julius Migos amesema shule hiyo ilikuwa na wanafunzi 808 wakati wa mkasa huo wa usiku wa kuamkia siku ya Alhamis 28, Mei 2026, ambapo bweni moja la wanafunzi wa shule hiyo lilishika moto na kuteketea.

Akizungumza na Wanahabari baada ya kutembelea shule hiyo, Waziri Migos alisema kati ya wanafunzi 79 waliyopata majeraha na kukimbizwa hospitalini, 71 kati yao walipokea matibabu na kuruhusiwa kuondoka na wazazi wao, wanafunzi wengine 7 wakiendelea kulazwa hospitalini.

Migos hata hivyo ameonya kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa mtu yeyote atakayepatikana amehusika katika mkasa huo wa moto kwenye shule hiyo ya Utumishi Girls Academy huku akiagiza kufungwa kwa shule hiyo kwa muda.

“Ningependa kusema kwamba sote tunajua kwamba mkasa huu umesababishwa na moto lakini uchunguzi ukikamilika na tubaini kwamba kuna watu walihusika iwe ni wanafunzi ama mtu binafsi serikali itamchukulia hatua kali zaidi”, alisema Migos

Naye Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen aliwataka wananchi kuwa utulivu na kuepuka kusambaza taarifa zisizo na uhakika mitandaoni kwani maafisa wa usalama bado wanaendelea na uchunguzi.

“Tunawataka wakenya wawe watulivu wakati uchunguzi ukiendelea na tutaeleza kila kitu baada ya kupata taarifa kamilifu kutoka kwa maafisa wetu wa upelelezi lakini sio vizuri kuweka mambo kwa mitandao na haujapata taarifa kamili,”alisema Murkomen.

Hata hivyo wazazi waliyofika katika shule hiyo wamependezeka mabweni yote katika shule mbalimbali nchini kuweka madirisha makubwa na milango mingi ili kuokoa maisha ya wanafunzi wakati wa mikasa ya moto sawa na sheria zilizowekwa na serikali kuhakikisha zinatekelezwa kikamilifu.

Maafisa wa Idara ya upelelezi wa jinai nchini DCI wamesema tayari wameanzisha uchunguzi ili kubaini chanzo cha mkasa huo wa moto katika shule hiyo ya upili ya wasichana ya Utumishi Girls Academy huko Gilgil kaunti ya Nakuru.