Kama njia mojawapo ya kuimarisha mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga, viongozi wa chuo Kikuu cha pwani kwa ushirikiano na Coco FM pamoja na wadau wengine wa mazingira walishiriki zoezi la upanzi wa mikoko katika kijiji cha Kibokoni wadi ya Kibarani kaunti ya Kilifi.
Naibu Chansela wa chuo kikuu cha Pwani Prof, James Kahindi pamoja na viongozi wengine wa chuo hicho ambao waliongoza zoezi hilo walisema walifanikiwa kupanda miche 2,500 huku wakieleza umuhimu wa kutunza mazingira.
“Zoezi la upanzi wa miche ni jukumu la kila mmoja kwani miti ni muhimu katika kuhakikisha kuna hewa safi na lengo letu kuu ni kupanda zaidi ya miche elfu kumi” alisema Kahindi.

Wadau wa masuala ya mazingira wasisitiza umuhimu wa upanzani wa miti kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa
Patience Manga Maramba ambaye alizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa chuo kikuu cha pwani aliwasihi wanafunzi wenza pamoja na vijana kujishughulisha na masuala ya utunzaji wa mazingira badala ya kuwaachia wazee na asasi husika kwani ni jukumu la kila mmoja kuyatunza mazingira.
“Ningependa kutoa wito kwa wanafunzi wenzetu kushiriki upanzi wa miche na sio kuachia wazee na asasi husika pekee” alisema Maramba
Nao baadhi ya wakaazi wa kijiji hicho cha Kibokoni walisema eneo hilo lilikuwa limeharibiwa kutokana na ukataji wa miti kiholela ila kupitia upanzi wa miche mazingira yameanza kuimarika tena na viumbe wa baharini wameanza kuongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Kwa upande wa maafisa wa shirika la uhifadhi wa misitu eneo bunge la Kilifi Kaskazini wakiongozwa na Uleo Stephen walitoa wito kwa wenyeji wa kaunti ya Kilifi pamoja na Wakenya kwa jumla kukumbatia upanzi wa miche na utanzaji wa mazingira na kutoa onyo kwa wale ambao wana hulka ya kukata miti kiholela.
Taarifa ya Janet Mumbi
