Jamii ya waumini wa dini ya Kiislamu mjini Malindi kaunti ya Kilifi wameombwa kuadhimisha sherehe za sikukuu ya Eid ul- Adha kwa kuwakumbuka wale wasio kuwa na uwezo.
Mwakilishi wadi ya Malindi mjini katika kaunti ya Kilifi Rashid Odhiambo alisema kila muumini wa dini yakiislamu ana jukumu la kuwasaidia wale wasiojiweza ili kujumuisha na wenzao katika kusheherekea sikukuu ya Eid-ul-Adha kwani ni mojawapo ya mwongozo wa dini ya kiislamu.

Waumini wa dini ya Kiislamu waungana na wengine kuswali swala ya Eid-ul-Adha
Akizungumza baada ya swala ya Eid, Odhiambo alitoa tahadhari kwa wazazi kutowaruhusu watoto wao kuzurura ovyo mitaani ili kuwaepusha kuvamiwa na wahuni wanaotumia sherehe hizi kwa uporaji hususan nyakati za usiku.
“Nawaomba wazazi wenzangu kuwa waangalifu na watoto wao wakati huu wa sherehe za sikukuu ya Eid-ul-Adha, kwa kuhakikisha wanafatilia mienendo ya watoto wao ili kuwapusha na visa potovu”,alisema Odhiambo
Odhiambo aliwataka wazazi kuandamana na watoto wao wanapozuru fuo za bahari kuogelea na kuhakikisha kuwa wanaogelea na watu wenye uzoefu wa kuogelea ili kuepeka visa vya wao kuzama maji ambavyo mara nyingi vimekuwa vikiripotiwa katika maeneo ya bahari hususan wakati wa sherehe.
