Serikali imekosoa maandamano yaliyoandaliwa siku ya Jumatatu Mei 18,2026 kote nchini ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta nchini.
Serikali imesema haitakubali baadhi ya watu kuendelea kuharibu na kupora mali ya umma, ikisema watakaopatikana watakabiliwa kikamilifu kwani maafisa wa kupambana na ghasia wako kila sehemu kuhakikisha usalama unaimarishwa pamoja na kulinda mali ya umma na biashara za wakenya.
Katika kikao na Wanahabari kilichojumuisha wakuu wa usalama nchini akiwemo Inspekta Jenerali wa polisi, Naibu Inspketa Jenerali wa polisi Eliud Lang’at, Katika katika Wizara ya usalama wa ndani Raymond Omollo miongoni mwa wengine, Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen alisema wakati wa maandamano hayo watu wanne walithibitishwa kupokeza maisha yao.
Waziri Murkomen alisema watu wengine 30 walijeruhiwa kufuatia makabiliana na maafisa wa polisi huku watu 348 wakitiwa nguvuni na kutokana na kushiriki maandamano ambayo hayajaidhinishwa na maafisa wa polisi.
“Ni jambo la kusikitisha kwamba watu wanne walipoteza maisha yao kufuatia maandamano hayo, lakini ningependa kuwaambia wananchi maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta haitasaidia, ni wadau wa sekta ya uchukuzi wa umma kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali na mwafaka utapatikana”, alisema Murkomen.
Murkomen pia aliwalaumu viongozi wa kisiasa nchini, akisema ndio wanaochangia taifa kushuhudia vurugu na maandamano ya kila mara hali ambayo taifa limekuwa likipoteza raslimali nyingi.
Aidha alieleza kwamba maandamano sio njia mwafaka ya kutatua tatizo la ongezeko la bei ya mafuta nchini huku akisisitiza kwamba serikali inalishuhulikia suala hilo kupitia ushirikiano wa Hazina ya kitaifa, pamoja na Wizara ya Kawi na Wizara ya uchukuzi na kwmaba wanaendelea na mikakati ya kuhakikisha suala hilo linatatuliwa kupitia mazungumzo na wadau wa sekta ya uchukuzi nchini.
