Bei ya Mafuta yapandisha joto la kisiasa nchini

Bei ya Mafuta yapandisha joto la kisiasa nchini

Mjadala kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli nchini Kenya unaendelea kushika kasi, huku wananchi wengi wakitaka maelezo ya kina kuhusu vigezo vinavyotumika kuongeza bei hizo karibu kila mwezi.

Wadau wengi wameonyesha wasiwasi wao kuhusu tofauti ya bei ya mafuta kati ya Kenya na mataifa jirani yasiyo na bandari kama Uganda, Rwanda na Burundi, hali ambayo imeibua maswali kuhusu mfumo wa uagizaji na usimamizi wa mafuta nchini.

Shinikizo hilo limechochea maandamano ya wahudumu wa matatu na baadhi ya washikadau wa sekta ya uchukuzi katika maeneo tofauti nchini leo Mei 18, huku baadhi ya barabara zikishuhudia usumbufu mkubwa wa usafiri.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha runinga nchini, Waziri wa Hazina ya Kitaifa, John Mbadi, alikosoa maandamano hayo akisema hayatoi suluhu ya kudumu kwa changamoto iliyopo.

Kwa mujibu wa Mbadi, hali ya sasa ya bei ya mafuta imeathiriwa kwa kiwango kikubwa na mvutano wa kimataifa unaohusisha Marekani, Israel na Iran, ambao umechangia kuyumba kwa soko la mafuta duniani.

“Maandamano haya hayawezi kushusha bei ya mafuta. Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala za kudhibiti gharama hizi,” alisema Mbadi.

Aidha, Waziri huyo aliwashutumu baadhi ya wanasiasa kwa kile alichodai ni kutumia suala la bei ya mafuta kujijenga kisiasa badala ya kutafuta suluhu ya pamoja.

Hata hivyo, serikali bado haijaweka wazi iwapo ongezeko jipya la bei limetokana na shehena mpya ya mafuta iliyowasili nchini mwezi Aprili au changamoto za kimkakati katika uhifadhi wa mafuta nchini Kenya.

Mbadi alisema serikali imekuwa ikitekeleza hatua mbalimbali za kupunguza makali ya ongezeko hilo, zikiwemo:

Kuagiza mafuta kutoka mataifa tofauti

Kutumia mfumo wa serikali kwa serikali (G-to-G)

Kupunguza baadhi ya ushuru wa mafuta

Kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)

Wakati huo huo, serikali imetangaza kikao cha dharura kitakachowakutanisha Waziri wa Kawi, Opiyo Wandayi, Waziri wa Barabara na Uchukuzi, Davis Chirchir, viongozi wa vyama vya uchukuzi pamoja na wadau wengine muhimu katika sekta hiyo.

Lengo la kikao hicho ni kutafuta mwafaka wa haraka wa kusitisha maandamano yanayoendelea huku serikali ikitafuta mbinu za muda mrefu za kudhibiti bei ya mafuta na kupunguza mzigo kwa wananchi.

Taarifa ya Elizabeth Mwende