Madereva mjini Kilifi walalamikia mafuta yenye Madini ya Sulphur

Madereva mjini Kilifi walalamikia mafuta yenye Madini ya Sulphur

Madereva nchini wanaendelea kulalamikia masaibu ambayo wanayapitia baaada ya serikali kutangaza kupunguza viwango vya ubora wa mafuta yanayouzwa nchini, kwa kuruhusu madini hatari ya Sulphur kuongezwa kwa kipindi cha miezi sita.

Mjini Kilifi kaunti ya Kilifi baadhi ya madereva wa magari ya uchukuzi wa umma wakiongozwa na Albert Saro ambaye alizungumza kwa niaba yao alilalamikia namna mafuta hayo yanavyoathiri magari hayo na kuwasababishia hasara kubwa.

“Tunapitia matatizo mengi sahii, maana magari yanaharibika ghafla tukiwa barabarani na tukipeleka kwa fundi tunaambiwa mafuta hayo ndiyo yanayosababisha” alisema Saro.

Saro pia alisema hali hiyo inawafanya wanaomiliki magari hayo ambao wengi wao walichukua mikopo ili kuyanunua kukadiria hasara kwani wanalazimika kutumia fedha nyingi wanapoyapeleka gereji.

Walitoa wito kwa wizara husika kuingilia kati na kutafuta suluhu la kudumu ili kuwaepusha na madhila hayo.

Haya yanajiri siku chache baada ya waziri wa biashara nchini Lee Kinyanjui kufika mbele ya bunge la seneti kutetea kupunguzwa kwa viwango vya ubora wa mafuta hayo, akisema hatua hiyo ilichangiwa na kuvamiwa kwa maghala ya mafuta nchini Iran na maeneo ya Ghuba

Taarifa na Janet Mumbi