Mihadarati ya thamani ya Ksh. 2.19M imenaswa Mombasa

Mihadarati ya thamani ya Ksh. 2.19M imenaswa Mombasa

Maafisa wa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya mjini Mombasa wamefanikiwa kuwakamata washukiwa wawili wanaodaiwa kuhusika na usambazaji wa mihadarati yenye thamani ya shilingi milioni 2.1.

Washukiwa hao, Mwanaisha Abdalla Gona mwenye umri wa miaka 42 na Nancy Njeri mwenye umri wa miaka 37, walikamatwa katika operesheni ya pamoja katika eneo la Kwa Hola huko Changamwe kaunti ya Mombasa.

Maafisa wa DCI wamesema operesheni hiyo ilifanikishwa baada ya kupokea taarifa za kijasusi ambapo polisi walipata misokoto 902 ya bangi iliyokuwa tayari kuuzwa, na gramu 300 za Heroini, huku thamani ya dawa hizo ikikadiriwa kuwa shilingi milioni 2.19.

Vifaa vingine vilivyopatikana ni pamoja na mizani ya kidijitali na mifuko ya plastiki ya kufungia dawa hizo, hali inayodokeza kuwa washukiwa hao walikuwa wakihusika katika mtandao wa usambazaji wa Mihadarati.

Washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Chaani, wakisubiri kufikishwa Mahakamani huku maafisa wa DCI wakisema wataendelea kuwasaka wahusika wa biashara ya dawa za kulevya ili kukomesha mtandao huo.

Taarifa ya Mwanahabari wetu