Walimu tarajali waandamana Kilifi

Walimu tarajali waandamana Kilifi

Walimu tarajali wa sekondari msingi kaunti ya Kilifi wameandamana kuishinikiza serikali kuu kupitia tume ya kuajiri walimu nchini,TSC kutekeleza agizo la mahakama la kuwapa ajira ya kudumu.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya kuandamana hadi katika afisi za TSC Mjini Kilifi, wakiongozwa na Mwenyekiti wa kitaifa wa walimu tarajali, Nehemiah Kipkorir waliapa kusitisha huduma zao kikamilifu ikiwa ahadi yao ya kuondolewa kwenye ajira ya kandarasi haitekekezwa.

Walisema mshahara wa shilingi elfu 17 ambao wanalipwa hautoshi kukidhi mahitaji yao ya kila siku licha ya wengi wao kufanya kazi katika mazingira magumu.

“Serikali haijakuwa ikijali maslahi yetu na tunataka kulipwa mshahara mkubwa na pia tupewe kandarasi ya kudumu” Walisema walimu tarajali.

Ni kauli ambazo ziliungwa mkono na Khamis Chivatsi Mwarabu, naibu mwenyekiti wa KUPPET tawi la Kilifi akisema walimu wanahangaika kupata huduma za matibabu kutokana na ukosefu wa bima ya afya na pia kuilaumu KNEC  kwa madai kukosa kuwalipa walimu fedha zao baada ya kusaihisha mitihani ya KPSEA, KJSEA na KCSE.

“Walimu wanateseka hata kupata huduma za matibabu kutokana na ukosefu wa bima ya afya” Alisema Mwarabu.

Naye Penina Kadzo Baraza wa masuala ya jinsia kwenye muungano wa KUPPET kaunti ya Kilifi alisema walimu tarajali wanakumbwa na msongo wa mawazo kutokana na changamoto ambazo wanazipitia na kuitaka serikali kuingilia kati ili kupatikane suluhu la kudumu.

Taarifa ya Janet Mumbi