Serikali kusambaza neti milioni 10 kwa wananchi kuzuia Malaria

Serikali kusambaza neti milioni 10 kwa wananchi kuzuia Malaria

Kenya inatarajia kusambaza neti za kuzuia Mbu milioni 10 kwa wananchi mashinani huku Wizara ya Afya nchini ikiimarisha juhudi za kudhibiti maambukizi na vifo vinavyotoka na ugonjwa wa Malaria.

Katibu katika Idara ya Afya ya umma nchini Mary Muthoni amesema Malaria bado ni changamoto kubwa kwa Afya ya umma, akisema visa milioni 4.2 vilirekodiwa mwaka wa 2024.

Muthoni alisema kuna haja ya kushirikisha kila mmoja katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya Malaria nchini, akiwataka wananchi kusafisha mazingira yao ili kuwa na mazingira safi na salama kwa maisha yao.

“Tunapanga kusambaza zaidi ya vyandarua vya kuzuia Mbu milioni 10 kote nchini, kama hatua moja wapo ya kuzuia maambukizi ya Malaria na vifo kwani ugonjwa wa Malaria umekuwa changamoto kuu nchini”, alisema Muthoni.

Kwa upande wake mkuu wa mpango wa Malaria katika Wizara ya Afya nchini Dk Kibor Keitany alisema kiwango cha mamabukizi ya malaria nchini kimeshuka hadi asilimia 6 mwaka wa 2020 kutoka asilimia 8 mwaka wa 2025.

Keitany alisema mpango huo unalenga kupunguza Malaria kwa asilimia 80 na kupunguza vifo vinatokana na ugonjwa huo kwa asilimia 90.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi