Wapwani waonywa dhidi ya mafuriko

Wapwani waonywa dhidi ya mafuriko

Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini imetangaza kuendelea kushuhudiwa kwa vipindi vya mvua katika sehemu mbali mbali nchini kuanzia siku ya Jumatano Aprili 22 hadi tarehe 27 mwezi huu wa Aprili.

Idara hiyo ilitangaza kwamba viwango vya mvua vitaongezeka hadi milimita 20 katika muda wa saa 24 katika eneo la Pwani sawa na Kaskazini na Kusini Mashariki mwa nchi.

Miongoni mwa kaunti zitakazoathirika na mvua hizo ni pamoja na kaunti za Kwale, Mombasa, Taita-Taveta, Kilifi, Tana River, Lamu, Garissa na maeneo ya kaunti za Wajir, Mandera, Kitui na Makueni.

Idara hiyo imeonya wakaazi kusalia waangalifu hasa katika maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko sawa na kutahadharisha kuhamia maeneo salama ili kuapuka majanga.

Katika taarifa iliyotumwa na idara hiyo kwa vyombo vya habari, ilisisitiza kwamba itakuwa ni hatua mwafaka iwapo wananchi watachukua tahadhari ya mapema na kujiepusha na mafuriko ambayo huenda yakashuhudiwa kutokana na mvua hizo.

Wakenya ambao wanaishi katika maeneo ya nyanda za chini wameshauriwa kuhamia maeneo salama ili kuepuka kusombwa na mafuriko ambayo mara nyingi husababishwa na mvua kubwa, huku ikizidi kuwarai wananchi kujiepusha kutembea maeneo ambayo yako na vidimbwi vya maji.

Idara hiyo pia iliwaonya madereva wa magari ya uchukuzi wa umma, kibinafsi na wale wa masafa marefu kuwa waangalifu wanapokuwa barabarani ili kuepuka utelezi wa magari ambapo mara nyingi husababisha ajali.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi