Kesi ya Mihadarati ya bilioni 8.2 kusikizwa Mahakama ya Mombasa

Kesi ya Mihadarati ya bilioni 8.2 kusikizwa Mahakama ya Mombasa

Kesi ya usafirishaji wa dawa za kulevya zenye thamani ya shilingi bilioni 8.2 iliendelea kusikilizwa katika mahakama ya Shanzu, shahidi wa pili ambaye ni afisa wa Jeshi la Wanamaji nchini akielezea mahakama kuwa jahazi lililokamatwa likiwa na dawa hizo halikuwa na utaifa wowote.

Akitoa ushahidi mbele ya Mahakama, Meja Mohamed Abdulrahman alisema chombo hicho kilikuwa kikifuatiliwa kwa muda mrefu na idara za kijasusi kutokana na tuhuma za usafirishaji wa mihadarati katika eneo la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.

Kwa mujibu wa ushahidi, jahazi hilo lililojulikana kama MV Igor lilikamatwa umbali wa maili 350 kutoka pwani ya Mombasa likiwa halina bendera wala nyaraka zozote za usafirishaji.

Mahakama pia ilielezwa kwamba meli hiyo ilihusishwa na tukio la kushusha mzigo unaoshukiwa kuwa wa dawa za kulevya katika mji wa Maputo nchini Msumbiji mnamo Juni mwaka 2025.

Katika operesheni hiyo, maafisa wa wanamaji walikamata watu sita wanaodaiwa kuwa raia wa Iran na kupata bidhaa nyeupe inayoshukiwa kuwa dawa za kulevya ikiwa imehifadhiwa kwenye makasha madogo.

Vifaa vingine vilivyopatikana ni pamoja simu tano za rununu, simu ya setilaiti, kadi za utambulisho zenye maandishi ya Kiarabu pamoja na kadi za benki na laini kadhaa za simu.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa huku Mahakama ikitarajiwa kutembelea makao makuu ya Jeshi la Wanamaji kushuhudia vielelezo vilivyokamatwa.

Taarifa ya Mwanahabari wetu