Shambulio la Osotsi lazua wasiwasi kwa upinzani

Shambulio la Osotsi lazua wasiwasi kwa upinzani

Seneta wa  Vihiga Godfrey Ososti anaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Karen jijini  Nairobi baada ya kusafirishwa kwa ndege jana Jumatano April 8 2026 kutoka mjini Kisumu, siku moja tu baada ya Naibu Kinara huyo wa Chama cha ODM, kuvamiwa na kundi la vijana waliojihami kwa silaha hatari mjini Kisumu.

Viongozi mbali mbali hasa kutoka upande wa upinzani nchini Kenya, wamekuwa wakitoa kauli kali za kushtumu shambulio hilo wakihoji nia na dhamira ya shambulio hilo.

 Osotsi ni miongoni mwa Viongozi wanaoasi Chama cha Odm katika mrengo wa Linda Mwananchi, wakiongozwa na Seneta wa Nairobi ambaye pia ni Katibu wa chama hicho Edwin Sifuna.

 Wakiongozwa na Knara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, walisema shambulio hilo dhidi ya seneta Osotsi huenda ni njama na vitisho kwa kusudi la kuzua uhasama baina ya jamii mbili za eneo la magharibi mwa nchi.

Kalonzo alisema viongozi wa kisiasa hasa wa upinzani wanafaa kupewa uhuru na mazingira salama ya  kuuza sera zao za siasa sawa na viongozi wengine serikalini, huku akishinikiza serikali kuhakikisha wahuni hao wanakamatwa na kukabiliwa kisheria.

Kiongozi huyo wa upinzani aliongeza kusema, iwapo serikali haitachukua hatua za haraka basi watalazimika  kumfungulia mashtaka Waziri wa usalama wa ndani Kichumba Murkomen na Katibu katika Wazira hiyo Raymond Omollo.

Viongozi wa kisiasa washutumu shambilio la kivamizi dhidi ya Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi

Kauli yake iliungwa mkono na Kinara wa chama cha DAP-Kenya Eugine Wamalwa ambaye alisema wahuni wamekuwa wakishambulia viongozi wa upinzani mara kwa mara jambo linalohatarisha usalama wa viongozi.

Katika kanda ya video iliyonaswa kwenye kamera za siri za CCTV siku ya Jumatano, kundi la vijana lilionekana likiingia kwenye mghahawa mmoja kisha kumshambulia na kumjeruhi seneta huyo.

Wakati huo huo Seneta wa Kakamega Bonny Khaluale aliitaka idara ya upelelezi nchini kuzamia suala la uvamizi dhidi ya viongozi unaotekelezwa na vijana wanaoonekana kukodishwa ili kuwanyamazisha wapinzani.

Taarifa ya Joseph Jira