Maafisa wa sekta ya uchukuzi wameahirisha mgomo wao baada ya mazungumzo yaliyoongozwa na Rais William Ruto katika ikulu ya Mombasa.
Maafisa hao wakiongozwa na rais wa Muungano wa wamiliki wa matatu Albert Karagacha wamesema kuwa mengi ya masuala waliokuwa nayo ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta nchini yameangaziwa kwa kina na rais Ruto.
Karagacha amewataka wahudumu wa sekta ya uchukuzi wa umma pamoja na wamiliki wa magari ya uchukuzi wa mizigo kuhakikisha wanarudisha magari yao barabarani, akisema masuala waliowasilisha kwa rais yameangaziwa
Akizungumza mda mfupi baada ya kufanya kikao na rais William Ruto mjini Mombasa, Karagacha amesema serikali imekuwa kiangazia kwa kina masuala mbali mbali yanayohusu sekta ya uchukuzi nchini.
Aidha amesema iwapo bado serikali itakuwa inajikokota katika kufanikisha masuala waliojadiliana basi wataitisha mazungumzo zaidi na Wizara husika ili kuafikiwa kwa ajenda zao huku akisema japo suala la mzozo wa mafuta sio jambo la Kenya pekee lakini taifa inawajibu wa kusaidia wananchi wake.
Wakati huo huo Karagacha amewataka wakenya kutoingiza siasa katika suala la kupanda kwa bei ya mafuta nchini.
Taarifa ya Joseph Jira
