Mudavadi apinga ripoti ya kikosi maalum cha Kenya nchini Haiti kuhusika na ubakaji

Mudavadi apinga ripoti ya kikosi maalum cha Kenya nchini Haiti kuhusika na ubakaji

Serikali imepinga ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu tuhuma za ubakaji dhidi ya maafisa wake wanaohudumu nchini Haiti chini ya Ujumbe wa kimataifa wa usaidizi wa usalama wa kimataifa.

Katika barua iliyotumwa kwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres tarehe 7 Aprili, Waziri wa masuala ya kigeni wa Kenya Musalia Mudavadi alielezea wasiwasi wake kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono na dhuluma ambayo yaliripotiwa Agosti 2025.

Mudavadi alisema madai hayo yalichunguzwa mara moja kupitia Bodi ya uchunguzi na kupatikana kuwa hayana uthibitisho kwani hakukuwa na malalamishi yaliyowasilishwa kwa mamlaka yoyote na kwamba matokeo yaliwekwa wazi na mashirika ya Haiti na Umoja wa Mataifa hayakuwa na uthibitisho.

Mudavadi aliongeza kuwa wafanyakazi wa MSS walifuata kikamilifu mifumo yote ya uendeshaji na kwamba hakuna ripoti zilizobainisha utovu wa nidhamu.

Ripoti ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi Februari na kuwekwa hadharani mwezi Aprili inaeleza kwamba maafisa chini ya ujumbe unaoongozwa na Kenya nchini Haiti walihusishwa katika visa vinne vya unyanyasaji wa kingono, kisa kimoja kikihusisha mtoto wa miaka 12.

Ripoti hiyo inasema madai hayo yalithibitishwa na uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa. Kulingana na Umoja wa Mataifa madai hayo yanachunguzwa. Haijabainika iwapo maafisa hao ni raia wa Kenya.

Ujumbe unaoongozwa na Kenya, uliotumwa Haiti mwaka 2024 kusaidia kukabiliana na ghasia za magenge, kufuatia idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, sasa nafasi yake imechukuliwa na Kikosi cha Kukakabiliana na Magenge.

Taarifa ya Elizabeth Mwende