Bajeti ya taifa yaongezeka hadi shilingi trilioni 4.6

Bajeti ya taifa yaongezeka hadi shilingi trilioni 4.6

Huenda wakenya wakalazimika kuingia mifukoni mwao hata zaidi ili kugharamia bajeti ya taifa ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026 ambayo inakadiriwa kufikia shilingi trilioni 4.6.

Bajeti hii imeongezeka na shilingi bilioni 363 kutokana na bunge la kitaifa kuidhinisha bajeti ya zaidi ili kukidhi mahitaji ya serikali licha ya bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2024/2025 kuwa shilingi trilioni 4.3.

Japo wakenya wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa gharama ya maisha wakiwa na matumaini ya kushuka kwa bajeti ya taifa ili kuwawezesha kukidhi mahitaji yao, matumaini hayo yameanza kupotea kutokana na mikakati ya kiuchumi iliyoidhinishwa na serikali ya Kenya kwanza.

Akizungumzia kuhusu ongezeko la bajeti hiyo kwa shilingi bilioni 363, Mwenyekiti wa Kamati ya bajeti katika bunge la kitaifa Samuel Atandi alisema fedha hizo za zaidi zitasaidia baadhi ya idara za serikali nchini ambazo zimekuwa zikikabiliwa na upungufu wa fedha.

Atandi ambaye pia ni mbunge wa Alego Usonga alidokeza kwamba sekta zilizoongezewa fedha ni pamoja na sekta ya Afya, Elimu na usalama wa taifa, akisisitiza kwamba suala hilo halifai kuchukuliwa kisiasa na badala yake litazamwe kama suala muhimu nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya bajeti katika bunge la kitaifa Samuel Atandi, akieleza bajeti ya taifa ya shilingi trilioni 4.6 ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026

Kwenye ongezeko hilo la shiling bilioni 363, sekta ya afya nchini imeongezewa mgao wa shilingi bilioni 26, ambapo sasa itapata mgao wa shilingi bilioni 164, Tume ya huduma kwa walimu nchini TSC ikiongezewa shilingi bilioni 24 na kufikia shilingi bilioni 411, Idara ya usalama nchini ikiongezwa shilingi bilioni 53 na kufikia shilingi bilioni 418.

Hata hivyo kamati hiyo imeeleza wazi kwamba kwenye mgao wa idara ya usalama, shilingi bilioni 10 zitaelekezwa kwenye idara ya ujasusi nchini, shilingi bilioni 7.5 kwenye idara ya polisi na shilingi bilioni 24 kwa idara ya ulinzi nchini, ili kufanikisha usalama wa taifa.

Wakati huo huo Atandi alikiri kwamba wakenya watahusishwa kikamilifu katika kutoa maoni yao kuhusu mapendekezo ya bajeti hiyo ya shilingi trilioni 4.6 ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026.

Kwa upande wake Waziri wa hazina ya kitaifa John Mbadi alisema wakenya watakuwa na fursa ya kutoa maoni yao kuhusu mapendekezo ya bajati hiyo ya taifa, akiwataka wanasiasa kujitenga na tabia ya kuchochea wakenya na kuvurugu masuala muhimu yanayohusu mwananchi.

Kulingana na kauli ya Kamati ya bajeti katika bunge la kitaifa, idara nyingi za kiserikali nchini zimekuwa zikitegemea kipengele cha 223 cha Katiba kuitisha fedha za dharura bila idhinisho la bunge la kitaifa na kwamba hatua hiyo imeonyesha wazi utumizi mbaya wa raslimali za umma.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi