Serikali imefanikiwa kutekeleza asilimia 55 ya mageuzi ya polisi

Serikali imefanikiwa kutekeleza asilimia 55 ya mageuzi ya polisi

Katibu katika Wizara ya usalama wa ndani Raymond Omollo amesema serikali imefanikiwa kutekeleza asilimia 55 ya mageuzi yanayoendelea ya kitaifa katika idara ya polisi nchini.

Omollo alisema kufuatia mkutano wa ngazi ya juu na kamati ya uongozi ya usalama wa kitaifa ulioongozwa na rais  William Ruto iliafikia kutekelezwa kwa mageuzi hayo kwenye idara ya polisi nchini.

Omollo alidokeza kwamba mchakato huo unalenga kuimarisha taasisi za kiusalama, kuboresha utoaji wa huduma na kuboresha mifumo ya polisi nchini.

“Tuko asilimia 55 ya mageuzi yanayoendelea ya kitaifa katika idara ya polisi nchini na kwamba juhudi hizo zitachangia kuimarisha idara ya polisi nchini sawa na kuhakikisha maafisa wa polisi wanapata mazingira bora na salama ya kufanya kazi”, alisema Omollo.

Omollo alisema kumekuwa na maendeleo ya kuridhisha katika maeneo muhimu, ikiwemo mageuzi ya kiutawala, kisheria na ustawi wa ndani ya huduma ya polisi na kwamba mabadiliko ya kimuundo na kiutendaji yanaendelea kutekelezwa.

Aidha, alisema serikali imeanza kutekeleza mareboresho ya mishahara ya polisi, huku awamu ya pili ya marekebisho ya mishahara ikitarajiwa ndani ya miezi miwili ijayo kabla ya utekelezaji kamili.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi