Serikali yahimizwa kufidia wakaazi wa Owino Uhuru

Serikali yahimizwa kufidia wakaazi wa Owino Uhuru

Shirika la kimazingira la Center for Justice Governance and Environmental Action limetoa makataa ya siku 30 kwa serikali kutekeleza uamuzi wa Mahakama ya juu wa kulipa fidia ya shilingi bilioni 1.3 kwa jamii ya Owino Uhuru kaunti ya Mombasa.

Hii ni kufuatia uamuzi huo ambao ulitolewa zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo Phyllis Omido alisema ni hali ya kusikitisha kuona hadi kufikia sasa serikali haijatekeleza agizo hilo la Mahakama licha ya madhara makubwa yaliyowapata wenyeji wa eneo hilo kutokana na sumu ya Lead kutoka kwa kiwanda ambacho kilikuwa kimejengwa eneo hilo.

Omido alisema kutotengwa kwa fedha hizo katika makadirio ya nyongeza ya bajeti ya mwaka wa 2025/26 yaliyowasilishwa bungeni tarehe 3 Machi mwaka huu kunaonyeshwa kupuuzwa kwa amri hiyo ya Mahakama.

Baadhi ya watu katika kijiji cha Owino Uhuru walifariki dunia kutokana na sumu hiyo na wengine kusalia na madhara mengi ya kiafya.

Taarifa ya Mwanahabari wetu