Shirika la kutetea haki za binadamu la Vocal Africa limeeleza wasiwasi wake kuhusu kukamatwa na kuendelea kuzuiliwa kwa Mwabili Mwagodi, katika kituo cha polisi cha Bandari kaunti ya Mombasa.
Kulingana na mkurugenzi wa shirika hilo Hussein Khalid, Mwagodi alihamishwa hadi kituo cha polisi cha Bandari baada ya kukamatwa awali katika eneo la Lungalunga karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania.
Khalid, alisema Mwagodi alikuwa akielekea Tanzania kufuatilia madai yake ya malipo kutoka kwa mwajiri wake wa zamani aliponaswa mpakani na kuzuiliwa.
Khalid alisema maafisa wa polisi hawajatoa taarifa rasmi za kukamatwa kwake, wakidai kwamba walikuwa wakitekeleza amri kutoka juu huku akiongeza kwamba Mwagodi anasubiri kusafirishwa hadi Nairobi.
Kwa upande wake dadake Mwagodi alisema maafisa wa polisi katika eneo la Lungalunga baadaye walimhamisha ndugu yake baada ya kudai kuwa hawakuwa na msingi wa kisheria wa kuendelea kumshikilia.
Kufikia sasa idara ya usalama haijatoa maelezo ya kina kuhusu madai hayo.
Taarifa ya Joseph Jira
