Kinara wa Chama cha Democratic Party (DP) Justine Muturi ameibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuhitilafiana na sajili ya wapiga kura kufuatia makubaliano kati ya tume huru ya uchaguzi na mipakani nchini IEBC na data ya sajili ya kitaifa ya watu NRB.
Muturi, alihoji kwamba makubaliano kati ya tume ya IEBC na NRB ambayo iko chini ya ofisi ya rais kuhusu kushirikiana na taarifa za data ni njama ya uwezi wa kura, akisema ataweka wazi suala hilo kwa umma.
Muturi alisema kuna taarifa kwamba afisa mkuu mtendaji wa tume ya IEBC Moses Sankuli amekuwa akifanya mikutano ya siri na maafisa wa sajili ya kitaifa ya watu NRB ili kubaini data kamili na pia amekuwa kishirikiana na kampuni binafsi za kieletroniki kama vile Smartmatic.
Kiongozi huyo alisema makubaliano yeyote yasio na uwazi yanayohusisha ofisi ya rais, hasa katika masuala yanayohusu taarifa za usajili wa wapiga kura na hifadhi data, yanatishia uadilifu, kuaminika na uwazi wa mchakato wa uchaguzi.
Akijibu tuhuma hizo, mwenyekiti wa tume ya IEBC Erastus Ethekon alisema mipango ya kushirikisha data na taasisi za umma za kibinafsi hufanyika chini ya mifumo madhubuti ya kisheria ili kuzuia udanganyifu, huku washirika wakipewa taarifa mara tu mchakato huo unapokamilika.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
