Mtihani wa KCSE waendelea vyema baada ya vurugu katika shule ya upili ya Malindi

Mtihani wa KCSE waendelea vyema baada ya vurugu katika shule ya upili ya Malindi

Baada ya kushuhudiwa vurugu na uharibifu wa mali ya shule katika Shule ya upili ya wavulana ya Malindi, hali imerejea kama kawaida na wanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo wanaendelea na mitihani yao ya kitaifa ya KCSE.

Hii ni baada ya watahiniwa wa kidato cha nne katika shule hiyo kutofautiana na mwalimu mkuu kuhusu mazingira tata, hali iliyosababisha uharibifu wa mali ya shule hiyo uliyotekelezwa na wanafunzi hao.

Naibu Chifu wa Shella mjini Malindi Nichodemus Mwayele, alisema wanafunzi hao walimshinikiza Mwalimu mkuu wa shule hiyo kuwaruhusu kuendelea kujitayarisha kwa mitihani yao katika sehemu ambayo haijaruhusiwa.

Mwayele alifichua kuwa hatua hiyo ndio ilipelekea wanafunzi kuzua vurugu na kuharibu mali ya shule hiyo ikiwemo Camera za siri CCTV, kung’oa Solar miongoni mwa vifaa vyengine, hali iliyosababisha maafisa wa usalama kuingilia kati.

“Kulikuwa na vurugu na rabsha katika shule hii lakini tulitatua hiyo na sasa wanafunzi wanaendelea na masomo yao kama kawaida, hizi vurugu zilichangiwa na wanafunzi kumlazimisha walimu mkuu kuwaruhusu mahali ambapo wanafunzi walikuwa hawaruhusiwi ndio maafisa wa uslaama wakaja kutuliza vurugu hizo”, alisema Naibu chifu.

Kwa upande wake Sarah Wambui mmoja wa wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo, aliwataka wanafunzi hao kuzingatia nidhamu na kujiepusha na vurugu ili kuepuka kufutiliwa mbali kwa mitihani yao ya kitaifa.

“Tunawaambia wanafunzi watulie wafanye mitihani yao kwa amani lakini wakiendelea kuzua vurugu basi huenda mitihani yao itasitishwa na sisi kama wazazi hatutaki hivyo, tunataka wanafunzi wafanye vizuri masomoni.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi