News
Murkomen:Dumisheni amani siku ya Sabasaba
Waziri wa usalama wa kitaifa Kipchumba Murkomen ameshinikiza amani wakati wa maandamano ya kumbukumbu ya siku ya Sabasaba ambayo inafanyika Julai 7, 2025.
Akizungumza katika kaunti ya Meru, Murkomen alieleza wasiwasi wake kuhusiana na matukio ya vurugu ambayo yameshuhudiwa wakati wa maandamano ya hivi karibuni, ambapo mali ya umma ikiwemo vituo vya polisi na majengo ya mahakama vilivamiwa na kuteketezwa moto.
Murkomen aliweka wazi kuwa majukumu ya polisi ni kulinda raia japo hawatakubali matukio ya ghasia na vurugu.
Vile vile waziri huyo alihimiza polisi kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha maandamano yaliyopangwa Julai 7 2025 yanakuwa ya amani.
Wakati huo huo huduma ya kitaifa kwa polisi nchini NPS ilionya kuhusu matukio yeyote ya kihuni wakati wa maandamano ya sabasaba.
Katika taarifa NPS iliahidi kutekeleza majukumu yake ya kuweka amani na kulinda raia huku ikitahadharisha kuwachukulia hatua kali watakaovunja sheria wakati wa maandamano hayo.
Taarifa ya Joseph Jira