Sports
Mshambuliaji wa Liverpool, Hugo Ekitike, Aitwa Timu ya Taifa ya Ufaransa kwa Mara ya Kwanza
Mshambuliaji wa Liverpool, Hugo Ekitike, ameitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kuchukua nafasi ya Rayan Cherki aliyejeruhiwa, Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) lilitangaza hapo jana.
Kabla ya mchezo wa Jumapili dhidi ya Arsenal, Ekitike alikuwa ameanza vyema maisha yake mapya Liverpool, akifunga mabao matatu katika mechi tatu za mashindano tangu kujiunga msimu huu wa joto akitokea Eintracht Frankfurt.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 pia alifunga mabao matano katika mechi tano akiwa na timu ya vijana ya Ufaransa chini ya miaka 21 msimu uliopita. Hata hivyo, Ekitike aliachwa nje wakati kocha Didier Deschamps alipotangaza kikosi cha Ufaransa kitakachocheza michezo ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Ukraine nchini Poland Ijumaa na dhidi ya Iceland mjini Paris Septemba 9.
Kwa upande mwingine, Cherki, ambaye hakupatikana Jumapili kwa klabu yake Manchester City kwenye Ligi Kuu ya England, anasumbuliwa na jeraha la msuli wa paja la kushoto (quadriceps), FFF lilithibitisha.
“Hatacheza kwa takribani miezi miwili,” alisema kocha wa City Pep Guardiola Jumapili baada ya kikosi chake kufungwa 2-1 na Brighton.
Matukio ya mwishoni mwa wiki pia yameacha Deschamps na changamoto nyingine.
-
Ousmane Dembele, aliyetupia mara mbili wakati Paris Saint-Germain ikiilaza Toulouse kwenye Ligue 1 Jumamosi, alitoka uwanjani akishika paja lake la kushoto.
-
William Saliba, ambaye alikosa mashindano ya Nations League Final Four mwezi Juni, aliondoka dakika ya tano tu kwenye mechi ya Arsenal dhidi ya Liverpool baada ya kugongana na Ekitike.
-
Ibrahima Konate, beki mwingine wa Ufaransa anayekipiga Liverpool, pia alitolewa nje dakika ya 79 baada ya kuonekana kulemaa.