News
Miraj awahimiza Wapwani kujisajili katika SHA
Seneta mteule Miraj Abdillahi amewasihi wakaazi wa kaunti ya Mombasa kujisajili katika bima ya Afya ya jamii SHA.
Akizungumza katika eneo bunge la Mvita, Miraj alisema bima hiyo ina manufaa mengi hasa kwa wale ambao wanaugua magonjwa sugu kama ya Saratani na kuwaonya wale ambao wanasusia bima hiyo.
Abdillahi alisema usajili katika bima hiyo ni hatua muhimu ya kuhakikisha kila mkenya anapata huduma bora za matibabu.
“Bima ya SHA ni muhimu sana katika kupata huduma za matibabu na ikiwa kila mmoja atajisajili itakuwa vyema ili kutibiwa bila changamoto zozote’’, alisema Miraj.
Abdillahi pia aliwataka viongozi walioko maeneo ya mashinani kushirikiana na wizara ya afya nchini ili kuwahamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa bima hiyo ya SHA.
Taarifa ya Janet Mumbi