News

LSK yamtaka Inspakta Kanja kuweka wazi kifo cha Ojwang’

Published

on

Chama cha mawakili nchini LSK kinamtaka Inspakta jenerali wa Polisi nchini Douglas Kanja kuhakikisha kuna uwazi kufuatia kifo tatanishi cha mwanablogu Albert Ojwang’.

Akihutubia Wanahabari siku ya Jumatatu, rais wa LSK Faith Odhiambo alimwagiza Kanja kutangaza majina ya maafisa ambao wanazuiliwa wakiwemo wale waliomsafirisha Ojwang’ kutoka kaunti ya Homabay hadi jijini Nairobi.

Kanja alitangaza kuzuiliwa kwa maafisa polisi waliokuwa zamu katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi wakati Ojwang’ alipowasilishwa kituoni ambapo baadaye alipatikana akiwa na majeraha mabaya ndani ya seli.

Odhiambo aliongeza kuwa taarifa iliyotolewa na Inspakta Jenerali Douglas Kanja kuhusu kifo cha mwanablogu huyo haitosheleza kufafanua yaliyojiri.

“Kwa nini hajataja majini ya maafisa waliozuiliwa? Mbona anaficha? Wacha wakenya wafahamu. Tunataka kujua maafisa waliomchukuwa Ojwang’ je wao ni miongoni mwa wanaozuiliwa?”, alisema Odhiambo.

Rais huyo wa LSK pia alilaumu jinsi maafisa wa usalama walivyomshikilia Ojwang’ hadi akakutana na mauti yake

“Jinsi walivyomhudumia Albert Ojwang’ ni ukiukaji wa haki zake pamoja na wananchi wakenya. Hiki hakiwezi kuchukuliwa kama kisa cha kawaida kwa sababu kinaashiria namna mamlaka inavyohudumu ndani ya huduma ya maafisa wa polisi”, aliongeza rais wa LSK.

Wakati huo huo waanadamanaji pamoja na wanaharakati walikusanyika nje ya makafani ya City jijini Nairobi wakishinikiza hatua za haraka kuchukuliwa kuhusiana na kisa hicho.

Taarifa ya Joseph Jira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version