News

Kimotho: Deni lililosalia kwa waathiriwa wa bwawa la Mwache ni shilingi bilioni 2

Published

on

Serikali imesema itakamilisha malipo ya fidia kwa waathiriwa wote wa ujenzi wa mradi wa Bwawa la Mwache katika eneo la Kinango kaunti ya Kwale ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Katibu katika Idara ya unyunyizaji maji nchini Ephastus Kimotho amesema deni lililosalia kwa waathiriwa wa mradi huo ni shilingi bilioni 2 na tayari limeanza kulipwa.

Kimotho amesema hatua hiyo imeafikiwa baada ya Tume ya kitaifa ya ardhi NLC kupewa shilingi milioni 600 ambazo zitapewa waathiriwa kama fidia kuanzia wiki ijayo.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo sawa na kuzindua kituo cha afya cha Mazeras kinachojengwa kama sehemu ya mradi huo, Kimotho amesema fedha zilizosalia zitaanza kutolewa kuanzia mwezi Julai ili kuafikia mipango iliyowekwa.

“Kufikia mwezi Julai mwaka huu tutakuwa tumeanza kusambaza mgao mwengine wa fedha zilizosalia ili kukamilisha fidia hizo kufikia mwezi Disemba mwaka huu”, alisema Kimotho.

Shughuli za ujenzi wa Bwawa la Mwache

Kwa upande wake Gavana wa Kwale Fatuma Achani amesema mradi huo uko na manufaa mengi kwa wakaazi wa kaunti ya Kwale ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, shule, miongoni mwa manufaa mengine.

“Tumeona manufaa mengi kupitia mradi huu, umeleta vituo vya afya karibu na wananchi, ujenzi wa shule za Chekechea na miradi mingi muhimu ya umma, hivyo basi tunafaa kuunga mkono kikamilifu”, alisema Gavana Achani.

Mradi huo ambao ulikuwa umetengewa shilingi bilioni 4.6 kama fidia ya wakaazi waliopeyana ardhi zao kwa ujenzi wa mradi huo zimekuwa zilipiwa kwa njia ya awamu hali ambayo ilisababisha maandamano kutokana na kucheleweshwa kwa fidia hiyo.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version