News
Wahudumu wa Sekta ya Uchukuzi Wanahimiza Ukarabati wa Barabara ya Kibaoni-Ganze-Bamba
Wahudumu wa sekta ya uchukuzi mjini Kilifi kaunti ya Kilifi wanashinikiza serikali kuu na ile ya kaunti kuzingatia ukarabati wa barabara ya Kibaoni-Ganze hadi Bamba licha ya kushinikizwa kusitisha maandamano ya kufunga barabara hiyo.
Wakizungumza na Coco FM, wahudumu hao wamesema barabara hiyo ingali na hitilafu nyingi na wanahofia huenda ikaharibika vibaya msumu huu wa mvua.
Wakiongozwa na Praise Majimbo ambaye ni mhudumu wa bodaboda, wamesema hatua ya kulima barabara hiyo kwa tinga tinga haitoshi kwani bado kuna vumbi na mashimo hali inayowatatiza shughuli zao za kibiashara.
“Kwa sasa kidogo iko na afadhali lakini bado hatujaridhika na kile chenye tunapitia, kwa sababu kwengine kushatengenezwa na mvua imenyesha tayari sasa hivi mashimo yako mengi, vyenye niko tayari nyewe nimechoka kutoka Kakanjuni mpaka barabara vyenye iko kwa ukweli, vumbi na mashimo pia yashaongezeka kwa sababu ya mvua”, alisema Majimbo.
Nao wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma wakilongozwa na Samson Kitsao Wako, wanasema wanapitia changamoto za kukarabati magari yao kila mara kutokana na hali mbaya ya barabara hiyo.
“Lakini kwa saa tutasema inaafadhali kwa sababu, tuliandamana na tukafunga na baadaye serikali ikaleta tinga tinga ikapiga msasa kutoka hapa Kibaoni mpaka Silala, lakini sasa kutoka Ganze mpaka Bamba ndio barabara ni mbaya sana, mvua ikianza kunyesha tutapata shida sana kwa sababu barabara wakati wa mvua hua inateleza”, alisema Kitsao.
Vile vile wachuuzi wa vyakula kando ya barabara hiyo Wakiongozwa na Fiki Kenga wanasema idadi ya wateja imekuwa ikipungua kutokana na vumbi linalotoka barabarani kila mara, wakisinikiza serikali kuzingatia kilio chao.
“Tunapata taharuki hata vyakula vyetu huwa haviendi vizuri kila siku, hii barabara ilifanya kukwaruzwa kwaruzwa huko, angalau tusiumizwe na hili vumbi, barabara iko na vumbi wateja wanalalamika kwa sababu vumbi si nzuri kwa chakula, kwa hivyo tunaomba msaada tuwe nasi tutakaa vizuri mahali tuko”, waliongeza baadhi ya wachuuzi.
Aidha wameshinikiza serikali kuangazia matatizo wanayopitia baadhi yao wakidai wanawake wajawazito wamekuwa wakipoteza watoto wachanga hasa wanaposafirishwa kwa pikipiki kuelekea hospitali kujifungua kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
Itakumbukwa kwamba wakaazi pamoja na wahudumu wa uchukuzi wa umma waliandamana na kufunga barabara hiyo kwa majuma kadhaa na kutatiza shughuli za usafiri.