News
Nassir, Awaonya Vijana Wanaojihusisha na Uhalifu Mombasa
Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir amekashifu vikali ongezeko la vijana wadogo wanaoendeleza uhalifu katika kaunti hiyo.
Abdulswamad amewakosoa wale wanaosema kuwa vijana hao wanatekeleza uhalifu kutokana na ukosefu wa ajira, akisema wengi wa vijana hao ni wa umri mdogo.
Aidha amekariri kuwa vijana walio chini ya umri wa miaka 18 hawawezi kupewa ajira, akisema ni sharti wazazi wawajibike katika malezi ya watoto wao ili kuwaepusha dhidi ya utovu wa maadili.
Kauli yake imeungwa mkono na Mwenyekiti wa baraza la kitaifa la ushauri kwa waislamu KEMNAC, Sheikh Juma Ngao ambaye amesema wazazi wengi wamezembea katika kuwalea watoto wao hali inayowasababishia vijana hao kujiingiza katika uhalifu.
Sheikh Ngao amependekeza vijana hao wakamatwe na wachukuliwe hatua kali za kisheria pasi na kujali umri wao.