News
Kesi ya Wakili Joseph Munyithia na Farid Salim Yachukua Mkondo Mpya
Kesi ya wizi wa ardhi inayomuhusisha Wakili Joseph Munyithia na mfanyabiashara Farid Salim Almaary imechukua mkondo mpya.
Hii ni baada ya mwanasheria huyo kuandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Makupa mjini Mombasa akijitenga na madai ya wizi wa kipande hicho cha ardhi kilichoko katika eneo la Shelly Beach eneo bunge la Likoni.
Katika taarifa yake kwa Polisi, Munyithia ameeleza kwamba alishughulikia ardhi hiyo ambayo alikabidhiwa hatimiliki na Gabriel Mutiso ambaye kwa sasa ni marehemu.
Aidha ameeleza kwamba mnamo Machi tarehe 4 mwaka 2024 alipeana cheti cha kukodisha shamba hilo pamoja na barua ya uhamisho hadi kwa kampuni ya J Katisya and Co Advocates.
Wakili huyo mkuu katika kampuni ya Munyithia, Mutugi na Umazi Advocates ameandikisha taarifa takriban wiki moja baada ya ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini ODPP, kuagiza kukamatwa kwake pamoja na mfanyabiashara Farid.
Munyithia pamoja na mfanyabiashara huyo wanadaiwa kuiba na kuficha hati miliki ya ardhi hiyo kulingana na malalamishi yaliowasilishwa na wamiliki wa shamba hilo.