County
Mabunge Kupeperusha Mijadala Mbashara, Kumsaidia Mpwani Kuelewa Hoja
Ili kuhakikisha wakaazi wa kaunti za Pwani wanafahamu kinachojadiliwa na kupitishwa katika mabunge ya kaunti ni vyema iwapo mabunge hayo yatawekeza mbinu za kisasa za kiteknolojia na kupeperusha mijadala yao moja kwa moja.
Kulingana na Mwanaharakati wa maswala ya kisiasa Dan Owino Aluar, Wajumbe katika mabunge ya kaunti wamekuwa wakijifungia katika mabunge hayo bila ya kujadili maswala msingi yanayomhusu mwananchi.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa, Owino amesema wajumbe hao hawataki kuweka wazi wanayoyajadili kwani kazi yao kubwa ni kupigia debe magavana wa kaunti zao ili wanufaike kisiasa, akisema mabunge hayo yanafaa kupeperusha mijadala yote ya bunge kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Kauli sawa na hiyo imetolewa na mkereketwa wa maswala ya kisiasa katika eneo la Changamwe Samuel Chaka ambaye amesema kama inavyofanyika katika bunge la kitaifa na seneti, mabunge ya kaunti hayana budi ila kufuata mkondo huo.