Mahakama Kuu nchini imesitisha kwa muda mpango wa serikali ya Marekani na Kenya wa kuanzisha kituo cha karantini cha Ebola humu nchini.
Jaji wa Mahakama hiyo, Patricia Nyaundi, ameagiza kusitishwa kwa muda kwa utekelezaji wa makubaliano hayo hadi pale kesi iliyowasilishwa Mahakamani itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Katika uamuzi wake, Jaji Nyaundi alisema Kenya pia hairuhusiwi kupokea mtu yeyote aliyekumbana na Ebola au aliyeambukizwa ugonjwa huo chini ya mpango huo hadi kesi hiyo itakapomalizika.
Shirika la kutetea haki za kiraia la Katiba Institute liliwasilisha kesi hiyo mahakamani likipinga mpango huo siku hiyo hiyo ulipotangazwa.
Shirika hilo limesema kuanzishwa kwa kituo hicho kwa siri na bila ushirikishwaji wa umma kunazua maswali mengi kuhusu haki za maisha, afya, uwajibikaji wa serikali na usimamizi wa bunge.
Kabla ya kesi hiyo kuwasilishwa Mahakamani, Serikali ya Marekani kupitia Rais Donald Trump ilikuwa imekubaliana na Kenya na kutangaza mpango wa kuwahifadhi kwa muda raia wake waliokumbana na virusi vya Ebola nchini Kenya.
Hatua hii ililenga kuzuia ugonjwa huo kuingia katika ardhi ya Marekani, ambapo sasa mpango huo umekumbana na kikwazo kikubwa baada ya Mahakama kuu nchini kusimamisha kwa muda mpango huo.
Kwa mujibu wa Ikulu ya White House, raia wa Marekani waliokuwa katika maeneo yenye mlipuko wa Ebola lakini hawajaonyesha dalili za ugonjwa huo walitarajiwa kuwekwa katika kituo maalum cha karantini katika Kambi ya Anga ya Laikipia mjini Nanyuki.
Maafisa wa utawala wa Marekani walikuwa wamesema wale ambao wangepata dalili za Ebola hawangerejeshwa Marekani, bali wangepelekwa katika nchi nyingine kwa matibabu ya juu zaidi.
Hatua hiyo ilionekana kuwa mabadiliko makubwa ya sera ikilinganishwa na milipuko ya Ebola iliyopita ambapo wagonjwa Wamarekani waliruhusiwa kurejeshwa nyumbani kwa matibabu.
Lengo la mpango huo lilikuwa kuhakikisha hakuna kisa cha Ebola kinachoingia nchini Marekani.
