Chama cha Jubilee kimemkosoa vikali Katibu Mkuu wa chama cha UDA, Hassan Omar, kufuatia matamshi yake yaliyomhusu Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.
Viongozi wa Jubilee wakizungumza katika mkutano wa wajumbe wa chama uliofanyika Kiambu, walisema kauli za Hassan Omar zinaweza kuchochea uhasama wa kikabila na kuhatarisha mshikamano wa kitaifa.
Akihutubia wanachama katika hafla hiyo, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta aliikosoa serikali ya Kenya Kwanza kwa kile alichodai ni kulegeza nidhamu miongoni mwa viongozi wake wanaotoa matamshi ya uchochezi hadharani.
Uhuru aliwakumbusha Wakenya kuhusu athari za migawanyiko ya kisiasa na kikabila, akirejelea matukio ya mwaka 2007, na kusisitiza umuhimu wa kulinda amani na umoja wa taifa.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Naibu Kinara wa Jubilee, Fred Matiang’i, ambaye alisema chama hicho hakitakubali kuona kiongozi wao akidhalilishwa kisiasa.

Wajumbe wa Chama cha Jubilee wakongamana kuangazia mikakati ya chama kabla ya uchaguzi mkuu, 2027
Matiang’i alisisitiza kuwa Uhuru Kenyatta alitekeleza majukumu yake kama rais kwa uwezo wake wote akiwa madarakani, na viongozi wa sasa wanapaswa kuelekeza nguvu katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi badala ya kulaumu waliotangulia.
Wakati huo huo, licha ya Hassan Omar kuomba msamaha na kueleza kuwa matamshi yake hayakulenga jamii ya Wakikuyu, shinikizo dhidi yake linaendelea kuongezeka. Baadhi ya viongozi wa UDA pamoja na wananchi sasa wanamtaka kujiuzulu kutokana na kauli hizo zilizozua mjadala mkubwa wa kisiasa nchini.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
