EPRA yatangaza ongezeko la bei ya mafuta

EPRA yatangaza ongezeko la bei ya mafuta

Madereva nchini sasa watalazimika kulipa zaidi kwa mafuta baada ya Mamlaka ya kudhibiti bei ya Petroli nchini EPRA kutangaza ongezeko la bei za mafuta kwa kipindi cha Mei 15 hadi Juni 14, 2026.

Katika mabadiliko mapya yaliyotangazwa usiku wa kuamkia leo, EPRA imeeleza kuwa gharama ya Super Petroli na Dizeli imeongezeka kwa shilingi 16.65 na shilingi 46.29 kwa lita.

Jijini Nairobi, Super Petroli, Dizeli na mafuta ya taa sasa itauzwa kwa shilingi 214.25, shilingi 242.92 na shilingi 152.78 mtawalia kwa siku 30 zijazo.

Jijini Mombasa, Super Petroli, Dizeli na mafuta ya taa sasa zitauzwa kwa shilingi 211.09, shilingi 239.64 na shilingi 149.49 mtawalia.

EPRA imesema kuwa marekebisho hayo yanaakisi kupanda kwa bei za bidhaa za petroli katika soko la kimataifa, pamoja na mabadiliko ya kiwango cha ubadilishaji wa fedha na utekelezaji wa ushuru wa kisheria, chini ya mfumo wa Kodi ya ongezeko la Thamani (VAT).

Kulingana na EPRA, Serikali itawasaidia watumiaji kupitia Mfuko wa ushuru wa maendeleo ya petroli (PDL) kwa kutumia takriban shilingi bilioni 5, kufadhili bei za Dizeli na mafuta ya taa.

Taarifa ya Joseph Jira