Awamu ya pili ya zoezi la uchaguzi wa viongozi wa mashinani wa chama cha UDA imefanyika katika kaunti 18 kote nchini.
Zoezi hilo lilifanyika katika kaunti 6 za pwani pamoja na kaunti za Kisumu, Siaya, Migori, Kisii, Bungoma, Makueni, Machakos, Kitui, Isiolo, Marsabit na Turkana ili kuwachagua viongozi wa mashinani wa UDA.
Wagombea wa nyadhifa mbali mbali walijitokeza katika zoezi hilo ambalo lilivutia umati wa watu katika baadhi ya vituo.
Baadhi ya wagombea walieleza kuridhishwa na utaratibu wa zoezi hilo huku baadhi wakilalamikia changamoto za kimitambo katika baadhi ya vituo hali iliyowaacha baadhi ya wapiga kura nje.
Katika kituo cha shule ya msingi ya Kilifi mjini Kilifi, baadhi ya wagombea walilalamikia kuchezewa shere na wenzao, baada ya orodha ya majina kubatilishwa na kusababisha mchanganyiko miongoni mwa wafuasi wao.
Viongozi wakuu ndani ya chama cha UDA akiwemo mwenyekiti wa bodi ya barabara nchini Aisha Jumwa alipiga kura katika wadi ya Kakuyuni kuchagua viongozi hao wa mashinani.

Mgombea wadhfa wa useneta katika kaunti ya Kilifi kwenye uchaguzi mkuu wa 2027 Wakili George Kithi akizungumza na wakaazi.
Hata hivyo wakaazi wengi walisema zoezi hilo lilifanyika bila ya hamasa ya kutosha.
Wagombea wengi walieleza imani na zoezi hilo katika harakati za kuongoza chama cha UDA kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Taarifa ya Joseph Jira
