Serikali ya kaunti ya Kilifi imebuni jopo la kuchunguza malimbikizi ya madeni ambayo yamedumu kwa muda mrefu bila ya wanakandarasi kulipwa zabuni zao.
Jopo hili lililoteuliwa na gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Maitha Mung’aro, linajukumu la kutathmini uhalali wa zabuni hizo huku kukiwa na shaka kuwa huenda baadhi ya kandarasi hizo zimetolewa kwa njia ya ulaghai.
Kaunti ya Kilifi ni miongoni mwa kaunti ambazo zinashtumiwa kwa malimbikizi ya madeni kwa wanakandarasi.
Bado kuna maswali mengi yanayokosa majibu kuhusiana na ongezeko la malimbikizi haya ya madeni ya kaunti ya Kilifi na utaratibu unaotumika kuwalipa wanakandarasi ambao sasa wanahoji ni vipi ulaghai huu ulivyotekelezwa pasi ya kuzingatiwa kwa utaratibu na mifumo ya kisheria katika utoaji wa zabuni.
Serikali ya kaunti ya Kilifi sasa inadaiwa takriban shilingi billioni 12 kwa mujibu wa ripoti ya hivi punde ya mkaguzi wa hesabu za serikali Nancy Gathungu.
Deni hilo linatokana na huduma za wanakandarasi ambao wametoa huduma kwa kaunti na baadhi yao wamekuwa wakidai pesa zao kwa zaidi ya miaka mitatu bila ya malipo.
Hali hii imetajwa kuchangia pakubwa kuzorota kwa uchumi wa kaunti ya Kilifi hasa ikizingatiwa mchango wa wafanyibiashara hao kwa uchumi wa kaunti.
Mbali na athari kubwa kwa uchumi na wanakandarasi wenyewe ni dhahiri kwamba miradi mingi ya maendeleo pia imekwama kutokana na makisio ya bajeti yasiyoendana na hali halisi ya mfuko wa bajeti wa kaunti.
Hivi majuzi Gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Maitha Mung’aro alifutilia mbali baadhi ya kandarasi na miradi ya maendeleo ili iweze kutathminiwa upya.

Uzinduzi wa ujenzi wa barabara za mashinani ulipewa wanakandarasi
Malimbikizi ya madeni haya ya mabilioni ya pesa pia yanatajwa kuchangia pakubwa msongo wa mawazo kwa baadhi ya wanakandarasi ambao wamejikuta wakiuziwa vyombo na mali zao ili kulipa mikopo waliotumia kufadhili kandarasi zao.
Hata hivyo wiki mbili zilizopita, kaunti ya Kilifi ilibuni Jopo maalum ya kuchunguza na kutathmini madeni hayo kabla ya kuidhinishwa kwa malipo.
Hali hii imeathiri kaunti nyingi ikiwemo kaunti yaĀ MachakosĀ ambako wanakandarasi wamelazimika kuandamana barabarani wakidai haki yao baada ya kusubiri malipo kwa muda nrefu.
Maandamano hayo yalipelekea maafisa wa usalama kutumia vitoa machozi kuwatawanya wanakandarasi hao huku baadhi yao wakikamatwa na kuwekwa korokoroni.
Taarifa ya Eric Ponda
