Kaunti ya Kilifi ni moja wapo ya kaunti 47 zinazokabiliwa na changamoto za dhulma za kijinsia, mimba za utotoni, umaskini, mila na tamaduni potovu na mifumo duni ya afya ya jamii.
Takwimu za hivi punde, zinatoa picha ya wasiwasi kwani kufikia Oktoba mwaka wa 2024, zaidi ya wasichana 7,000 katika kaunti ya Kilifi walikuwa wamejifungua wakiwa na umri mdogo.
Ingawa idadi hiyo ilipungua hadi takriban 4,500 mwaka huu, idadi hiyo inasalia kuwa kubwa mno na kuwafanya viongozi wa eneo hilo na watetezi wa watoto kutoa wito wa kuwepo kwa juhudi za haraka za kulinda wasichana wadogo na kutafuta suluhisio la kudumu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa STRIDES for SRHR through Resilient Health Systems (STRIDES) katika kituo cha Afya cha Ganze, kaunti ya Kilifi, Naibu Gavana wa Kilifi Flora Mbetsa Chibule alitaja hali hiyo kuwa ya kusikitisha sana.
“Kilifi, ni kati ya kaunti nyingi katika taifa letu, inaendelea kukabiliwa na changamoto za kipekee katika kuhakikisha kila kijana na kila mwanamke anafurahia haki ya kupata huduma bora za afya,” alisema Flora.

Mpango wa STRIDES for SRHR through Resilient Health Systems (STRIDES) katika kituo cha Afya cha Ganze
Aidha alielezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa visa vya unajisi na kujamiiana na watu wa ukoo, akiwaonya wahalifu wanaowadhulumu wasichana walio katika mazingira magumu, hasa kutoka kwa familia zenye umaskini.
Kulingana na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Aga Khan Kenya, Susan Otieno, mradi wa STRIDES ni ushirikiano wa miaka saba (2025–2032) wenye thamani ya takriban shilingi bilioni 2.3, unaofadhiliwa na Serikali ya Canada, zitasaidia pakubwa kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia kaunti ya Kilifi.
Mpango huo utatekelezwa kupitia muungano wa washirika ikiwemo Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), huduma za afya za Aga Khan (AKHS), Kituo cha kimataifa cha afya ya uzazi Kenya (ICRHK), na Moving the Goalposts (MTG)—kwa ushirikiano na Serikali ya kaunti ya Kilifi.
Mpango huo utalenga kaunti ndogo tano—Kilifi Kaskazini, Kaloleni, Rabai, Malindi, na Ganze kwa lengo la kupunguza mimba za utotoni, kupambana na dhulma za kijinsia na kuimarisha uhusiano kati ya jamii na vituo vya afya.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
