Waziri wa Elimu nchini Julius Migos amesema ana matumaini kwamba mgomo wa Wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma kote nchini utasitishwa hivi karibu.
Waziri Migosi alisema siku ya Jumamosi na Jumapili, Maafisa wa serikali, wadau wa sekta ya elimu na viongozi wa vyama vya Wahadhiri nchini walifanya mazungumzo ya faraga katika kaunti ya Machakos na ripoti rasmi itatolewa kwa umma.
Akizungumza na Wanahabari, Waziri Migos alisema mazungumzo hayo yanatarajiwa kuibuka na suluhu na huenda wiki hii shughuli za masomo katika vyuo vikuu vya umma zikarejea kama kawaida.
Waziri Migos, alidokeza kwamba Tume ya kutathmini mishahara na marupurupu ya wafanyikazi wa umma nchini SRC imetoa shilingi bilioni 7.2 kwa Wahadhiri kama malipo ya malimbikizi ya mkataba wa makubaliano wa CBA wa mwaka wa 2017-2021.
“Serikali, wadau wa elimu na viongozi wa vyama vya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini UASU walifanya mkutano kaunti ya Machakos kuzungumza kuhusu mgomo wa wahadhiri na tayari Tume ya SRC imetoa shilingi bilioni 7.2 kuma malipo ya malimbikizi ya mkataba wa makubaliano wa CBA wa mwaka wa 2017-2021, japo wahadhiri walikuwa wametaka shilingi bilioni 7.9”, alisema Migos.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
