Muungano wa upinzani nchini umekashfu vikali matamshi yaliyotolewa na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga dhidi ya kifo cha Hayati Raila Odinga.
Muungano huo kupitia Msemaji wao Dkt Mukhisa Kituyi ulijitenga na matamshi hayo ikitaka kiongozi huyo ambaye ni mwanachama wa UDA kuchukuliwa hatua za kinidhamu huku ukisema upinzani hauna tabia kama hizo.
Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Muungano huo wa upinzani, imelitaka baraza la magavana nchini kumchukulia hatua kali za kisheria Gavana Kahiga, ikisema matamshi yaliyotolewa na gavana huyo hayahusiani na upinzani.
Dkt Mukhisa alisema matamshi ya Gavana Kahiga yanalenga kuchangia chuki nchini pamoja na kukiuka pakubwa kipengele cha 33 cha Katiba ya Kenya huku akimtaka Rais William Ruto na viongozi wa UDA kujitokeza na kuomba msamaha kwa naiba ya Gavana huyo kuhusu matamshi aliyoyatoa.
Tayari Gavana Kahiga alijiuzulu kama Naibu mwenyekiti wa baraza la magavana pamoja na kuomba msamaha kutokana na matamshi aliyoyatoa kuhusu kifo cha Hayati Raila Odinga.
