Mahakama ya Kilifi imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja gerezani mwanaume wa umri wa miaka 30 kwa kosa la kuvamia na kumjeruhi mwenzake.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama hiyo Ivy Wasike amesema hukumu hiyo imezingatia uzito wa kesi hiyo na ushahidi wa pande zote uliotolewa mbele ya Mahakama kuhusu kesi hiyo.
Hukumu hiyo imetolewa baada ya kiongozi wa mashtaka Nancy Njeru kueleza Mahakama kwamba mshtakiwa Kelvin Fujo Magogo ana rekodi ya uhalifu wa wizi wa mifugo na kesi hiyo iko katika Mahakama hiyo.
Awali kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Mahakama ilielezwa kwamba mshtakiwa Fujo, mkaazi wa Madamani wadi ya S okoke eneobunge la Ganze kaunti ya Kilifi, mnamo tarehe 14 mwezi Juni mwaka 2022 mwendo wa saa saba usiku katika eneo la Kiwandani mjini Kilifi akitumia panga alimjeruhi mlalamishi Noah Karisa Kalume.
Mahakama hiyo vilevile ilielezwa kwamba mshtakiwa aliabiri pikipiki ya mlalamishi ili kupelekwa kwake ambapo baadaye aliingia ndani ya nyumba kuchukua nauli badala yake akatoka na panga na kumjeruhi mlalamishi ambaye aliokolewa na bodaboda mwenzake aliyekuwa akipita na kumfikisha hosipitalini kwa matibabu.
Mshtakiwa ameelezwa kuwa ana siku 14 za kukata rufaa iwapo hajaridhishwa na hukumu hiyo.
Taarifa ya Teclar Yeri
