Mahakama kuu imesitisha kwa mda sheria tata ya kudhibiti matumizi ya mtandao ya mwaka wa 2025 pamoja na matumizi mabaya ya kompyuta, iliyofanyiwa marekebisho bungeni na kutiwa saini na Rais William Ruto kuwa sheria, Oktoba 15.
Jaji wa Mahakam kuu ya Milimani Lawrence Mugambi, alitoa agizo hilo akisema kesi hiyo ina uzito na agizo hilo limetolewa ili kupeana nafasi ya kesi hiyo iliyowasilishwa Mahakamani na Mwanamziki wa injili Reuben Kigame na Tume ya haki za binadamu nchini KHRC, itakaposikizwa na kuamuliwa.
Walalamishi wa kesi hiyo, walidai kwamba vifungu vya sheria hiyo vinakiuka haki kadhaa za kikatiba, ikiwemo uhuru wa kujieleza, haki za kikatiba, utambulisho wa kidijitali usiojulikana na hatua za kiutawala za haki.
Katika hati kiapo cha kesi hiyo, walalamishi hao pia walidai kwamba sheria hiyo ina vipengele visivyoeleweka na kupita kiasi, ambayo vinaharamisha kujieleza mitandaoni na kudhohofisha sheria ya Kenya ya kulinda data 2019.
Walalamishi hao pia walionya kwamba hatua hizo zinatishia watetezi wa haki, Wanahabari na wakosoaji wa serikali, pamoja na kudhoofisha ulinzi uliowekwa chini ya sheria ya ulinzi ya taarifa za kibinafsi ya mwaka 2019.
Viongozi wa kidini hata hivyo walimkosoa rais Ruto kwa kutia saini sheria hiyo, wakisema itakandamiza uhuru wa kujieleza, kuondoa maudhui yaliyoangaziwa kwenye mtandao hasa inayokosoa serikali pamoja na kukosoa adhabu ambayo ilitolewa na serikali ya faini ya shilingi milioni 20 ama kifungo cha miaka 10 gerezani.
