Wakenya ambao bado hawajachukua Vitambulisho vya kitaifa wamehimizwa kutembelea Ofisi za Msajili wa Vitambulisho na vyeti vya kuzaliwa ili kutuma maombi ya kupata stakabadhi hiyo muhimu ya kitaifa.
Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen aliwarai wakenya kutodharau pendekezo hilo, akisema Rais William Ruto aliondoa ada zote zinazohitajika wakati wa kutuma maombi ya kupata stakabadh hiyo.
Murkomen alisema serikali imeondoa pia ada ya shilingi elfu moja kwa wale wanaopoteza Vitambulisho vyao, akisema Vitambulisho vya kitaifa vinatolewa bure kwa wanaochukua kwa mara ya kwanza na wale waliopoteza.
“Rais aliona kwamba wakenya wengi hawana uwezo kwa kulipia vitambulisho na akaondoa hiyo ada ya shilingi elfu moja kwa wale waliopoteza Vitambulisho vyao, na wale wanaotuma maombi kwa mara kwa ya kwanza pia nao hawatatozwa pesa yoyote, yani sasa kupata kitambulisho ni bure,” alisema Murkomen.
Waziri Murkomen alisema Vitambulisho vya kitaifa vitawasaidia wakenya kupata fursa ya kujisajili kama wapiga kura na kuwa na nafasi nzuri ya kutekeleza jukumu lao la kidemokrasia wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
