Mashirika ya kupigania amani Kenya yang’aa kwenye tuzo Tanzania

Mashirika ya kupigania amani Kenya yang’aa kwenye tuzo Tanzania

Mashirika ya Kenya ya kupigania amani katika jamii yameendelea kujizolea sifa na umaarufu katika taifa jirani la Tanzania baada ya kutuzwa kwenye mashindano ya mpango wa “Amani na Usalama- (IPSA)” mwaka 2025 yaliyoandaliwa jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Miongoni mwa mashirika yaliyotuzwa ni shirika la Re-Imagining New Communities ambalo limetuzwa kutokana na mchango wake wa kupigania mageuzi ya amani kupitia elimu ya amani na ushirikiano wa dini mbalimbali unaolenga watoto, walimu na wachungaji nchini Kenya.

Akipokea tuzo kwa niaba ya shirika hilo, Grace Wendo msimamizi wa mipango katika shirika hilo, alielezea ushindi huo kama “uthibitisho wa athari ambazo shirika limekuwa nazo tangu kuanzishwa kwake 2021.

“Nishani hii ni ya kila mtoto ambaye ameongoza mazungumzo katika maabara yetu ya amani, kila mwalimu ambaye amefanikisha mazingira ya darasa salama na la malezi, kila kiongozi wa kidini ambaye ametetea umoja, na kila jumuiya ambayo imechagua maridhiano badala ya migawanyiko”,  alisema Bi Wendo.

Shirika la Re-Imagining New Communities limekuwa nguvu inayoongoza katika ujumuishaji wa ujenzi wa amani Kenya.

Mtazamo wake unaozingatia mtoto huwapa vijana uwezo wa kuwa mawakala wa mabadiliko, wakati programu zake za kiimani na mazungumzo ya jamii hutengeneza majukwaa salama ya kushughulikia mizozo na kukuza mshikamano wa kijamii.

Bi Wendo alisisitiza kuwa utambuzi huo ni ukumbusho kuwa amani haijengwi na mtu mmoja mmoja, bali ushirikiano wa jamii.

Utambuzi huo unakuja katika wakati muhimu huku Jumuiya kote Afrika Mashariki zikiendelea kukabiliana na masuala ya migogoro, ubaguzi na ukosefu wa usalama.

Kwa kutwaa tuzo hiyo, Re-Imagining New Communities iliiweka Kenya mstari wa mbele katika juhudi za amani na usalama zinazoendeshwa mashinani, na hivyo kuimarisha mchango wa nchi katika ajenda pana ya amani ya Afrika.

“Huu sio mwisho wa safari yetu,” aliongeza Bi Wendo. “Ni wito wa kwenda mbali zaidi, kufikia jamii zaidi, na kuhakikisha kuwa amani inashikiliwa na kila mtoto na kila familia.”

Taarifa ya Joseph Jira