Sports
Napoli yatangaza kumsajili Rasmus Hojlund kwa mkopo kutoka Manchester United
Kilabu ya Napoli hapo jana imetangaza kumsajili mshambuliaji Rasmus Hojlund kwa mkopo kutoka kilabu ya Manchester United ikiwa na wajibu wa kumnunua kwa mkataba wa kudumu, hatua inayomaliza kipindi chake kigumu kwenye klabu ya Old Trafford.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza, Napoli italipa pauni milioni 38 (sawa na dola milioni 51.5) kwa mkataba wa kudumu wa Hojlund msimu ujao.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 raia wa Denmark alisajiliwa na United akitokea Atalanta miaka miwili iliyopita, lakini alihangaika kuthibitisha thamani ya ada yake ya pauni milioni 64 kwenye kikosi kilichokuwa kinakosa ufanisi. Alifunga mabao 26 katika mechi 95 za mashindano yote akiwa na miamba hiyo ya Ligi Kuu ya England, lakini aliachwa nje na kocha Ruben Amorim kabla ya kuanza kwa msimu huu.
Hojlund alipata wakati mgumu katika ligi ya Uingereza msimu uliopita, akifunga mabao manne pekee katika mechi 32, japokuwa alifunga mara sita katika safari ya United kufika fainali ya Europa League.
Napoli walihitaji mshambuliaji mpya baada ya Romelu Lukaku kujeruhiwa paja wakati wa maandalizi ya msimu, huku vyombo vya habari vya Italia vikidai anaweza kuwa nje hadi mwaka 2026.
Hojlund aliwahi kucheza Italia na Atalanta, akifunga mabao 10 katika mechi 34.
Kikosi cha Antonio Conte, Napoli, kilitwaa Scudetto kwa tofauti ya alama moja mbele ya Inter Milan msimu uliopita.
Napoli wameanza vyema kampeni ya kutetea ubingwa, wakishinda mechi zao mbili za mwanzo huku usajili wao mpya wa kiangazi Kevin De Bruyne akionyesha kiwango cha kuvutia.