News
Muturi, Amshutumu Rais Ruto Baada ya Kutimuliwa Kazini
Aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa umma nchini Justin Muturi amejitokeza na kupinga kauli ya Rais William Ruto aliyoitoa siku chache zilizopita kwamba alifutwa kazi kwa misingi ya kutowajibika kazini.
Muturi amesema kutimuliwa kwake kazini kulichangiwa na msimamo wake wa kuishinikiza serikali kupitia Rais Ruto kukomesha visa vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela nchini.
Katika kikao na Wanahabari jijini Nairobi, Muturi amesema hajutii kufutwa kwake kazi, akisema madai yaliyoibuliwa na Rais kwamba alikuwa haudhurii vikao vya baraza la mawaziri ni uongo mtupu kwani alikuwa amewasilisha maombi rasmi ya kutohudhuria vikao vya baraza la mawaziri.
Muturi amesema licha ya kushinikiza swala la utekaji nyara na mauaji ya kiholela nchini kukomeshwa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na idara husika bali tabia hiyo imekuwa ikiendelea, jambo ambalo sio mikakati ya ajenda ya Kenya kwanza.
Wakati huo huo amemshtumu rais Ruto akisema amekuwa akijitokeza hadharani na kutoa kauli za uongo kuhusu mikakati ya serikali ilhali hakuna mipango yoyote serikali ambayo rais Ruto anatekeleza.