News
Mhubiri tata Kipngeny Ametiwa Nguvuni Eneo la Chonyi
Maafisa wa Idara ya upelelezi nchini DCI wamemtia nguvuni Mhubiri tata Julius Kimtai Kipngeny wa Kanisa la Mlango wa Miujiza Deliverance katika eneo la Mishomoroni kaunti ya Mombasa.
Kulingana na maafisa hao, Mhubiri huyo amekamatwa akiwa na mifupa na vitu vingine vya maajabu akiwa katika kijiji cha Chonyi kaunti ya Kilifi pamoja na mwandani wake Baraka Tsuma mwenye umri wa miaka 32.
Maafisa hao wamesema Kipngeny na Tsuma walikuwa wakiendeleza ibada na kundi la wanawake kwenye ghofu la jumba hali ambayo iliwatia hofu maafisa hao.
Akithibitisha kutiwa nguvuni kwa Mhubiri huyo tata, Afisa wa Idara ya upelelezi wa jinai nchini DCI kaunti ya Kilifi David Siele amesema mifupa hiyo imepelekwa kwa uchunguzi wa kitaalam ili kuthibitisha iwapo ni mifupa ya binadamu au la.
Hata hivyo imebainika kwamba washirika wa Kanisa hilo ambalo anaongoza Mhuburi huyo tata ni wa jinsia ya kike pekee.