News
Mahakama ya Shanzu Imeagiza Mshukiwa wa Ugaidi Kuzuiliwa kwa Siku 14
Mahakama ya Shanzu katika kaunti ya Mombasa imeagiza mshukiwa wa kundi la kigaidi la Al-Shabab Ramadhan Mohammed Hassan kuzuiliwa kwa siku 14 zaidi ili kuwawezesha maafisa wa Idara ya upelelezi kukamilisha uchunguzi wao.
Mahakama imeelezwa kwamba Hassan alikamatwa katika eneo la Kichangii katika gatuzi dogo la Nyali kaunti ya Mombasa akiwa na vifaa vinavyodaiwa kutumiwa na kundi la Al-shabab kutekeleza mashambulizi.
Maafisa hao wa idara ya upelelezi wameeleza Mahakama kwamba simu ya mshukiwa ilipelekwa katika makao makuu ya kitengo cha kupambana na ugaidi nchini ATPU kwa uchunguzi zaidi.
Kulingana na maafisa hao, baada ya kufanya uchunguzi wa simu ya mshukiwa wamebaini kwamba mshukiwa alikuwa akiwasiliana na wanachama wengine wa kundi la kigaidi la Al-shabab ambao wako mafichoni katika mataifa ya Tanzania na Somalia.
Hata hivyo maafisa hao wameitaka Mahakama kutomuachilia mshukiwa huyo kwa dhamana, wakisema kwamba huenda akatoroka na kuathiri uchunguzi wa kesi hiyo, ombi ambalo Mahakama imelikubali.
Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 16 mwezi huu.