Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai nchini (DCI) wamemtia mbaroni mshukiwa mmoja katika eneo la Kazandani, kaunti ya Mombasa kwa tuhuma za matumizi yasiyofaa ya mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na DCI, mshukiwa huyo Halima Ngache, maarufu kama Princess Halima, amekamatwa baada ya uchunguzi kubaini kuwa anahusishwa na akaunti ya mtandao wa X, (Twitter), ambayo inadaiwa kuchapisha taarifa nyeti kuhusu mienendo ya watu wanaolindwa na serikali.
DCI imesema kuwa suala hilo linachunguzwa kama tishio linalowezekana kwa usalama wa taifa.
Kwa sasa, mshukiwa anazuiliwa na anaendelea kufanyiwa taratibu za kisheria kabla ya kufikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, DCI imewakumbusha wananchi kuwa ingawa Katiba inalinda uhuru wa kujieleza, haki hiyo inapaswa kutumiwa kwa uwajibikaji na kwa kuzingatia sheria ikiwahimiza wananchi kuepuka kusambaza taarifa zinazoweza kuhatarisha usalama wa watu wanaolindwa au kuchochea taharuki miongoni mwa umma.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
