Kaunti ya Lamu yaandaa jukwaa la kuangamiza ukame

Kaunti ya Lamu yaandaa jukwaa la kuangamiza ukame

Kaunti ya Lamu imeandaa Awamu ya Pili ya mkutano wa ngazi ya juu kwa ajili ya kuangazia mikakati ya kuangamiza ukame ambayo ni hatua muhimu kuelekea kuimarisha ustahimilivu wa muda mrefu na usimamizi wa kukabiliana na majanga katika kaunti nzima.

Mkutano huo ulioongozwa na Waziri wa Ardhi, maji na Nishati katika kaunti hiyo Tashrifa Abubakar, pamoja na wadau wa Mamlaka ya kitaifa ya kukabiliana na Ukame (NDMA) pia uliwaleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo mashirika ya serikali na washirika wa maendeleo.

Washiriki walielekezwa kuhusu vipengele muhimu vya mfumo wa awamu ya Pili ya kuangamiza ukame, unaolenga kuhamia kutoka hatua za dharura za kukabiliana na ukame kuelekea mifumo endelevu ya muda mrefu.

Washiriki wamethibitisha dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano chini ya muundo wa jukwaa la uratibu katika ngazi ya kaunti- CSG, wakitambua kuwa ni jukwaa muhimu la kupanga kwa pamoja, kufanya maamuzi, na kutekeleza mipango.

Mkutano huo pia ulitumika kama jukwaa la kusherehekea utambuzi wa kimataifa wa hivi karibuni wa Kaunti ya Lamu kupitia Tuzo za Kimataifa za Water Transversality, ambapo Mpango wa Uondoaji Chumvi na Usimamizi wa Maji wa Kiunga ulitunukiwa kama Mradi Bora wa Athari kwa Jamii (2026).

Viongozi wa kaunti ya Lamu pamoja na Mamlaka ya kukabiliana na ukame na washkadau mbalimbali wanafanya kikao cha kuangazia mikakati ya kudhibiti ukame

Mradi wa Kiunga ni mfano bora wa ustahimilivu jumuishi unaoongozwa na jamii.

Awali ulianzishwa kufuatia uhaba mkubwa wa maji uliosababisha migogoro ya rasilimali, suala ambalo liliwasilishwa kwa jukwaa la uratibu katika ngazi ya kaunti kwa majadiliano.

Viongozi wamesisitiza kuwa mafanikio ya mradi wa Kiunga na utambuzi wake wa kimataifa yalitokana moja kwa moja na uratibu madhubuti chini ya mfumo wa Jukwaa hilo, ukiungwa mkono na Mamlaka ya Kitaifa ya kukabiliana na Ukame-NDMA.

Kaunti hiyo imethibitisha nafasi yake kama mfano bora wa jinsi mbinu jumuishi za sekta mbalimbali zinavyoweza kushughulikia kwa ufanisi changamoto za ukame, migogoro, na mabadiliko ya tabianchi.

Taarifa ya Joseph Jira