Ofisi ya DPP yafungua kesi ya nne dhidi ya Mackenzie

Ofisi ya DPP yafungua kesi ya nne dhidi ya Mackenzie

Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma, DPP, amefunga rasmi kesi ya nne na ya mwisho inayohusiana na mauaji ya halaiki ya watu katika msitu wa Shakahola, ambapo Mhubiri tata Paul Mackenzie na washtakiwa wengine 94 wanakabiliwa na mashtaka 238 ya kuua bila kukusudia.

Hatua hiyo imekuja baada ya shahidi wa 95 wa upande wa mashtaka ambaye ni mkuu wa upelelezi wa mauaji, Inspecta mkuu Raphael Wanjohi kuieleza Mahakama namna mtuhumiwa mkuu alivyodhibiti wafuasi wake hadi kusababisha vifo vya watu 429.

Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkuu Alex Ithuku, Wanjohi alisema Mackenzie na wenzake walikuwa na makubaliano ya pamoja ya kile alichokiita “mkataba wa kujiua,” wakidai kuwa walihamasisha kufunga hadi kufa kwa kisingizio cha kukutana na Yesu kabla ya mwisho wa Desemba 2020.

Aidha alieleza kuwa washtakiwa walikuwa na nia ya pamoja ya kusimamia vifo vya watoto na watu wazima kupitia mfungo wa kulazimishwa, huku wakijua wazi kuwa walikuwa wakitekeleza kitendo kisicho halali, jambo linalodhihirishwa na namna walivyoficha makaburi.

Upelelezi ulibaini kuwa Mackenzie alikuwa na kundi la ulinzi lililodhibiti mienendo ya watu na kuhakikisha mfungo huo unatekelezwa kikamilifu, huku mawasiliano ya simu yakionyesha ushirikiano wa karibu kati yake na wasaidizi wake.

Taarifa ya Mwanahabari wetu